Ujerumani kuunga mkono kikosi cha Kenya cha kudumisha amani Haiti

Martin Mwanje
2 Min Read

Ujerumani imeahidi kuunga mkono kikosi cha usalama cha Kenya kitakachotumwa Haiti kudumisha amani nchini humo.

Aidha Ujerumani imeahidi kuunga mkono juhudi za kudumisha amani katika Upembe wa Afrika.

Ahadi hizo zilitolewa na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wakati wa mazungumzo kati yake na Rais William Ruto pembezoni mwa “Kongamano la Ushirikiano wa Nchi Zilizostawi Zaidi Kiuchumi Duniani, G20 na Afrika,” linalofanyika jijini Berlin.

Bunge la Kitaifa na lile la Seneti nchini Kenya tayari yameidhinisha kutumwa kwa maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti ili kurejesha usalama katika taifa hilo la Carribean ambalo limekuwa likihangaishwa na magenge ya wahalifu kwa muda.

Hata hivyo, utumwaji wa maafisa hao unasubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na chama cha Thirdway Alliance kinachopinga hatua hiyo.

Rais Ruto anasema Kenya inawajibu wa kujumuika na jumuiya ya kimataifa kurejesha amani nchini Haiti.

Hata hivyo, upinzani umepinga kutumwa kwa maafisa wa polisi nchini Haiti ukihofia usalama wao na kudai hatua itakakuwa mzigo kwa Kenya ambayo tayari inakabiliwa na changamoto si haba za kiuchumi.

Aidha, unaitaja hatua hiyo kuwa isiyokuwa na mantiki kwani Kenya inakabiliwa na changamoto mzo za usalama hasa kaskazini mashariki mwa nchi.

Serikali imesema Kenya haitagharimika kwa vyovyote kwa kuwatuma maafisa wa polisi nchini Haiti.

Share This Article