Ujenzi wa barabara ya kuunganisha Kenya na Sudan Kusini kuanza karibuni

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa barabara na uchukuzi nchini Kenya Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Sudan Kusini Simon Mijok Mijak wametangaza kwamba ujenzi wa barabara kuu ya kutoka Nadabal hadi Juba utaanza hivi karibuni.

Mji wa Nadabal uko Sudan Kusini karibu na mpaka wa Kenya katika eneo la Bonde la Ufa na lengo kuu la ujenzi wa barabara hiyo ni kuhakikisha usafiri rahisi kati ya nchi hizi mbili.

Akizungumza katika kikao na wanahabari jana baada ya kukutana na Mijak, Murkomen alisema kwamba benki ya dunia na ile ya maendeleo barani Afrika zimeonyesha nia ya kufadhili mradi huo.

Kulingana naye waliagizwa na marais wa nchi hizi mbili kuhakikisha kwamba jiji la Juba limeunganishwa na bandari ya Mombasa nchini Kenya kupitia barabara hiyo.

Mawaziri hao wawili Murkomen na Mijak wameahidi kuzuru eneo la mradi huo kujifahamisha ulikofikia na kutagusana na watu wa maeneo ya karibu.

Mijak kwa upande wake alisema barabara hiyo ni muhimu kwa kusafirisha bidhaa kutoka bandari ya Kenya huko Mombasa hadi Juba na kurahisisha pia usafiri wa raia wa nchi hizi mbili.

Murkomen alifanya mkutano na Mijak na ujumbe wake jana hapa Nairobi kukamilisha majadiliano kuhusu ujenzi wa barabara hiyo.

Hatimaye itaunganishwa na ile ya kutoka Juba kuelekea jijini Douala nchini Cameroon kupitia taifa la Central African Republic na hivyo kuunganisha Afrika Mashariki na Afrika Magharibi.

Share This Article