Uingereza yakodi ndege kuwaondoa raia wake Mashariki ya Kati

Tom Mathinji
2 Min Read
Uingereza yakodisha ndege kuwaondoa raia wake Mashariki ya kati.

Huku mashambulizi ya kijeshi yakiendelea kushuhudiwa Mashariki ya Kati, Serikali ya Uingereza imekodi ndege ya kibiashara kutoka Oman kuwasaidia raia wake wanaotaka kuondoka eneo hilo.

Ndege inatarajiwa kuondoka mjini Muscat leo Jumatano, Machi,4, 2026 saa tano usiku saa za nchi hiyo (19:00 GMT), na itawapa kipaumbele watu walio hatarini zaidi.

Raia wa Uingereza, wenzi wao na watoto wao walio chini ya umri wa miaka 18, wataruhusiwa kutumia ndege hiyo.

Ofisi ya Mambo ya Nje inasema raia wa Uingereza ambao wamejiandikisha kuwa wapo Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE na kwa sasa wako Oman wanapaswa kujaza fomu maalumu haraka iwezekanavyo, ikiwa wangependa kuabiri ndege hiyo.

Ofisi hiyo aidha imeomba watu kutofika uwanja wa ndege hadi watakapofahamishwa na Ofisi ya Mambo ya nje.

Inaongeza kuwa itaendelea kushirikiana na mashirika ya ndege kutafuta njia zaidi za kurejesha watu nyumbani.

Usafiri wa anga katika Mashariki ya Kati umetatizika sana tangu Jumamosi iliyopita, wakati Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi dhidi ya Iran na kumuua Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei.

Tangu wakati huo, Iran imelipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi katika kanda nzima, yakilenga kambi za kijeshi za Marekani zilizopo katika mataifa ya Kiarabu, lakini pia miundombinu ya kiraia na nishati.

Maelfu ya safari za ndege zimesitishwa na raia wengi wa Uingereza ambao wangependa kuondoka wamekwama katika eneo hilo.

Taarifa ya BBC

Share This Article