Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC) na ile ya kusini mwa Afrika (SADC) zimewateua waliokuwa Marais Uhuru Kenyatta (Kenya), Olusegun Obasanjo(Nigeria), na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, kuwa wapatanishi katika mchakato wa kuleta amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Viongozi hao walichaguliwa baada ya mchakato wa amani wa Nairobi na ule wa Luanda kuunganishwa.
Hatua hiyo iliafikiwa wakati wa mkutano wa pamoja wa viongozi wa nchi na serikali ulioongozwa na Rais wa Zimbabwe aliyepia Rais wa SADC na mwenzake wa Kenya aliyepia mwenyekiti wa EAC William Ruto.
Mkutano huo uliandaliwa Jijini Dar es Salaam, Tanzania, mnamo Februari 8, 2025, ili kutatua mgogoro wa kiusalama unaokumba Mashariki mwa DRC.
Kama sehemu ya mchakato huo, wakuu wa vikosi vya ulinzi Afrika Mashariki, walikutana Jijini Nairobi Februari 21, 2025, kupigia kurunzi hali ya kiusalama nchini DRC na mikakati ya kuikabili.
Mkutano sawia na huo uliandaliwa na wakuu wa vikosi vya ulinzi vya kusini mwa Afrika SADC Dar es Salaam, Tanzania. Mikutano hiyo iliambatana na maagizo yaliyotolewa na mkutano wa pamoja wa viongozi na nchi kuhusu juhudi za kuleta amani nchini DRC.
Baadhi ya maagizo yaliyotolewa ni pamoja na kusitishwa mara moja kwa vita bila masharti yoyote, utoaji wa misaada ya kibinadamu, kufunguliwa kwa njia za usambazaji misaada, kubuniwa mpango wa kupeleka vikosi vya usalama katika eneo la Goma na maeneo yaliyo karibu, na kufunguliwa mara moja kwa uwanja wa ndege wa Goma.
Uongozi wa pamoja wa EAC-SADC, umetoa wito kwa wahusika wote katika mzozo huo, wakiwemo M23 na makundi mengine yaliyojihami kusitisha mapigano mara moja mashariki mwa DRC.
Kuchaguliwa kwa viongozi hao watatu, kunapiga jeki mchakato wa upatikanaji amani mashariki mwa nchini, na upatikanaji wa suluhu la kudumu katika mzozo huo wa muda mrefu.