Utawala wa Uhispania umetangaza kwamba umemwondoa kabisa balozi wake kwenye ubalozi wa taifa hilo jijini Tel Aviv nchini Israel.
Ana Maria Salomon Perez ameondolewa kwenye ubalozi huo kufuatia kile kinachotajwa kuwa mzozo wa kidiplomasia.
Taarifa ya serikali ya nchi hiyo ilielezea kwamba hatua hiyo iliafikiwa kutokana na hali tete ya kisiasa kati ya Madrid na Tel Aviv.
Tatizo linaaminika kutokana na msimamo wa Uhispania wa kupinga hatua ya Marekani kwa ushirikiano na Israel kushambulia Iran.
Maafisa wa serikali ya Uhispania wanatetea msimamo huo wakisema utadhihirisha pingamizi za nchi hiyo dhidi ya kuendelezwa kwa mashambulizi hayo na athari zake kwa usalama wa kikanda.
Msemaji wa serikali ya Uhispania amesema nchi hiyo inaamini kuwa mazungumzo na diplomasia ndiyo suluhisho la kudumu kwa migogoro ya kimataifa, na wala sio matumizi ya nguvu za kijeshi.
Uamuzi wa kupunguza pakubwa shughuli katika ubalozi wa Tel Aviv, kulingana na msemaji huyo, ni ishara wazi ya kutoridhishwa kwa nchi hiyo na hali ya sasa ya mvutano na hatua za kijeshi zinazochochea mgogoro katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa tofauti za kisera kati ya Uhispania na Israel kuhusu namna ya kushughulikia mvutano unaohusisha Iran.
Hata hivyo, wadadisi wameonya kwamba mgogoro huo wa kidiplomasia unaweza kuathiri ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya mataifa hayo.