Uhalifu wa mitandaoni na uongozi mbaya ni tishio kwa ukuaji wa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo almaarufu SACCOs humu nchini.
Kamishna wa Vyama vya Ushirika David Obonyo amesema visa vya uhalifu vinavyolenga au kutumia kompyuta vimeongezeka katika vyama vya ushirika vya akiba na mikopo kutokana na ukosefu wa mifumo thabiti ya teknolojia.
“Hii ni changamoto kubwa katika vyama vinavyokabiliwa na changamoto za kifedha na vile ambavyo vinakabiliwa na mizozo ya uongozi,” alisema Obonyo.
Aliongeza kuwa changamoto za kiteknolojia zimesababisha mifumo katika vyama vya ushirika vya akiba na mikopo kusambaratika na kwa kiasi fulani wanachama kupoteza rasilimali zao.
Vyama kadhaa vinaendesha shughuli zake kwa kutumia mifumo ya teknolojia ya zamani lakini katika siku za maajuzi, mifumo hiyo imekabiliwa na hatari kutokana na matishio yanayochipukia.
“Hii inaziweka rasilimali za wanachama katika hatari kubwa,” aliongeza Obonyo.
Kulingana naye, walaghai wanaotumia teknolojia wameingilia kati utendakazi wa shughuli za vyama vya ushirika vya akiba na mikopo na kuiba rasilimali na hivyo kuwasababishia wanachama hasara kubwa.
Obonyo anasema kando na bodi nzima ya wakurugenzi, kuna haja ya kuweka mifumo thabiti ya uongozi, mathalan, kamati za ukaguzi na usimamizi. Anasema kamati hizo zitasaidia kuongeza ukaguzi wa shughuli za vyama hivyo.
Makamu mwenyekiti wa muungano wa vyama vya ushirika nchini, CAK David Mategwa amesema uhalifu wa mitandaoni ni tishio kubwa kwa ukuaji wa biashara ya vyama vya ushirika vya akiba na mikopo nchini.
“Mifumo kadhaa ya shughuli za vyama vya ushirika vya akiba na mikopo imedukuliwa na kusababisha kupotea kwa taarifa na rasilimali za wanachama,” alisema Mategwa.
Kulingana naye, ongezeko la uhalifu wa mitandaoni umeongezeka kutokana na ukosefu wa uelewa kwa upande wa wakurugenzi na usimamizi mkuu, suala ambalo linapaswa kuangaziwa.