Kituo cha kudhibiti na Kuzuia magonjwa barani Afrika,CDC, kimetangaza Ugonjwa wa Monkey pox (Mpox), kuwa dharura ya Afya ya Umma barani humu.
Wanasayansi kutoka kituo hicho cha Afrika CDC, walisema ugonjwa huo unasambaa kwa kasi sana barani Afrika, wakidokeza kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya maambukizi 13,700 na vifo 450 vimenakiliwa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
“Tunatangaza Mpox kuwa dharura ya Afya ya Umma barani Afrika,” alisema Jean Kaseya Mkuu wa CDC barani Afrika.
Kulingana na Mkuu huyo wa CDC Afrika Jean Kaseya, ugonjwa huo huenda ukaenea na kushindwa kudhibitiwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Mpox sasa imevuka mipaka na kuathiri maelfu katika bara letu, familia zimesambaratika, uchungu na mateso zimegusa maeneo mengi ya bara letu,” alisema Kaseya.
Kuligana na takwimu kutoka shirika la CDC Afrika, kufikia Agosti 4, 2024, visa 38,465 na vifo 1,456 vimenakiliwa tangu mwezi Januari mwaka 2022.
Shirika la Afya dunia WHO linatarajiwa kukutana kwa dharura leo Agosti 14, kujadili kusambaa kwa ugonjwa huo.
Mpox huambikuzwa kutoka kwa wanyama hadi binadamu na pia kugusana na mtu aliyeambukizwa.