Ugonjwa wa Kimeta wazuka nchini Uganda

Tom Mathinji
1 Min Read

Usafirishaji wa ng’ombe na uuzaji wa bidhaa za nyama umepigwa marufuku katika wilaya ya Kyotera, nchini Uganda baada ya kuzuka kwa ugonjwa wa Kimeta.

Kulingana na afisa wa afya wa wilaya hiyo Dkt. Edward Muwanga, ugonjwa huo hadi kufikia sasa umesababisha vifo vya watu 17, huku wengine 28 wakilazwa katika hospitali mbali mbali.

“Tumesitisha ulaji bidhaa zinatokona na mifugo, ikiwa ni pamoja na nyama, maziwa au siagi. Maduka yote ya kuuza nyama yamefungwa kwa sababu tunajaribu kuokoa maisha,” alisema Dkt. Muwanga.

Takriban ng’ombe 40 wanaaminika wamefariki kutokana na maambukizi ya ugonjwa huo, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Mamlaka ya afya ya Uganda ilithibitisha kuzuka kwa ugonjwa wa kimeta, Novemba 26.

Kimeta ni ugonjwa nadra lakini mbaya, unaoambukiza unaosababishwa na bakteria (Bacillus anthracis).

Binadamu huambukizwa ugonjwa huo wanapogusana na wanyama walio na ugonjwa huo.

TAGGED:
Share This Article