Ugomvi wa tumbaku wasababisha mauti Likuyani, Kakamega

Carolyn Necheza
1 Min Read

Polisi katika katika kijiji cha Plot Ten, eneo la Seregeya, kaunti ndogo ya Likuyani, kaunti ya Kakamega wanamzuilia mwanamume mmoja kwa tuhuma za kumuua rafiki yake kwa kumpiga kwa chuma, baada ya wawili hao kudaiwa kugombania tumbaku yenye thamani ya shilingi hamsini.

Kwa mujibu wa mzee wa mtaa wa kijiji cha Plot Ten, Jacob Mukangai, mshukiwa Francis Mushila aliwaambia maafisa wa polisi kuwa alimua rafiki yake, Vitalis Shidenye, mwenye umri wa miaka arobaini na miwili, baada ya marehemu kumdai tumbaku aliyokuwa amemtuma kumnunulia siku kadhaa zilizopita.

Hata hivyo, familia ya marehemu Shidenye, ikiongozwa na shemeji yake, Jane Khasoha, na mpwa wake, Everline Lihanda, imekanusha madai hayo na kueleza kuwa marehemu, ambaye alikuwa akiishi peke yake, alikuwa amepokea shilingi elfu kumi na moja kutoka kwa mnunuzi aliyenunua kutoka kwake kipande cha ardhi mapema mwaka huu.

Familia hiyo inadai kuwa mshukiwa alimuua mpendwa wao kwa nia ya kumpora fedha hizo.

Kwa sasa, familia na jamii ya eneo hilo kwa jumla inaitaka serikali ifanye uchunguzi wa kina ili kuhakikisha haki inatendeka.

Carolyn Necheza
+ posts
TAGGED:
Share This Article