Uganda na Tanzania zimefuzu kwa nusu fainali ya michuano ya mwaka huu kuwania kombe la CECAFA kwa chipukizi walio chini ya umri wa miaka 18.
Uganda wameongoza kundi B kwa alama 6 baada ya kuwalemea Sudan Kusini magoli 2 kwa bila katika mechi ya mwisho iliyochezwa Jumamosi adhuhuri.
Tanzania wamefuzu kwa nusu fainali baada ya kutoka sare ya bao 1 dhidi ya Zanzibar katika mchuano wa mwisho.

Tanzania na Zanzibar walitoshana alama, magoli ya kufunga na ya kufungwa, na ikabidi nidhamu itumike kuwatenganisha ndugu hao ndiposa Tanzania wakawahi tiketi.
Mashindano hayo yatachukua mapumziko Jumapili na Jumatatu, kabla ya kurejea kwa nusu fainali Jumanne, Kenya wakifungua ratiba dhidi ya Tanzania ugani Mamboleo kaunti ya Kisumu saa sita adhuhuri, kabla ya Uganda kumaliza udhia na Rwanda baadaye saa tisa katika uwanja uo huo.