Taifa jirani la Uganda limelaani vikali uharibifu uliosababishwa na moto uliozuka kwenye jengo la kibiashara la Uganda House jijini Nairobi jana Jumanne.
Jengo hilo linamilikiwa na Uganda.
Kwenye taarifa, Katibu Bagiire Vincent Waiswa amepongeza Idara ya Zimamoto ya Nairobi kwa kuchukua hatua za haraka na kuuzima moto huo.
“Kwa hivyo tunatoa wito wa utulivu na kuepukana na uvumi usiokuwa na maana na kukimbilia kukisia chanzo cha moto huo ili kuruhusu kuchunguzwa kwa kisa hicho,” alisema Waiswa katika taarifa leo Jumatano.
Jengo hilo linalopatikana kwenye barabara ya Kenyatta Avenue katikati ya jiji la Nairobi limekuwa likifanyiwa ukarabati kwa muda sasa na orofa ya sita ya jengo hilo ilitarajiwa kufunguliwa tena keshokutwa Ijumaa. Ni orofa ya chini peke yake iliyokuwa ikitumiwa na wafanyabiashara.
Ofisi za Ubalozi Mdogo wa Uganda zilikuwa kwenye orofa ya tatu ya jengo hilo kabla ya wafanyakazi kuondolewa ili kupisha ukarabati.
“ingawa kuna uharibifu mkubwa uliotokea kwenye jengo hilo, tunashukuru kuwa hakuna vifo vilivyoripotiwa au majeraha mabaya ambayo yametambuliwa hadi kufikia sasa. Ni muhimu pia kubaini kuwa hakuna mfanyakazi wa Kidiplomasia au Ubalozi Mdogo aliyekuwa kwenye jengo hilo wakati moto ulipozuka,” aliongeza Waiswa.
Kulingana naye, licha ya kisa hicho, uhusiano kati ya Kenya na Uganda unasalia thabiti.
Amesema ingawa Uganda inaunga mkono maandamano ya amani kama njia ya kuwasilisha lalama, inalaani vikali vurugu ambazo husababisha uharibifu wa mali.