Shughuli ya kufukua miili 14 katika kaburi la pamoja katika kaunti ya Kericho inatarajiwa kufanyika leo Jumanne.
Kaburi hilo liligunduliwa Jumapili iliyopita.
Ufukuaji huo unakuja wakati ambapo watu wawili wamekamatwa na polisi kuhusiana na kaburi hilo la pamoja lililopatikana katika kaunti ya Kericho.
Waliokamatwa ni Afisa wa Afya ya Umma katika kaunti ya Nyamira David Araka na mlinzi wa kaburi hilo Richard Towett.
Hata hivyo, kesi dhidi ya washukiwa hao huenda ikachukua muda mrefu kabla ya kuanza kusikizwa baada ya polisi kuiomba mahakama kuwapa siku 30 zaidi ili kukamilisha uchunguzi.
Ukweli unatarajiwa kubainika baada ya korti kutoa kibali kwa polisi kufukua miili hiyo na mpasuaji mkuu wa serikali kuifanyia uchunguzi wa DNA.
Maafisa wa kaunti ya Nyamira walikiri kusafirisha mili 13 Alhamisi iliyopita hadi kwenye eneo ilikozikwa miili hiyo.
Eneo hilo linasemekana kumilikiwa na Baraza la Makanisa nchini (NCCK) na limewekwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.