Idara ya Mahakama kamwe haitavumilia visa vyovyote vya ufisadi kuathiri utendakazi wa idara hiyo kwa Wakenya.
Ahadi hiyo imetolewa na Jaji Mkuu Martha Koome wakati ambapo kumekuwa na madai ya kushamiri kwa ufisadi katika idara hiyo.
Isitoshe, ombi la kutaka Jaji Koome na Majaji wenzake sita wa Mahakama ya Juu limewasilishwa kwa Tume ya Huduma za Mahakama, JSC kutokana na tuhuma za ufisadi.
“Sambamba na masuala ya utendakazi bora, pia tunakabiliwa na madai mapya ya ufisadi ndani ya baadhi ya vituo vyetu vya mahakama. Haya ni masuala yanayoibua mashaka mno na hatuwezi tukayapuuza,” amesema Jaji Koome katika hotuba yake iliyorekodiwa kwa njia ya video na kuchezwa wakati wa mkutano wa Majaji wa Mahakama ya Masuala ya Wafanyakazi leo Jumatatu.
“Nataka kusema kwa mara nyingine bila kutetereka kwamba idara ya mahakama ni mahali pasipokuwa na ufisadi. Na kama sote tunavyojua na tumeelezea hivyo katika makongamano mengi na hata kwenye mpangokazi wetu, tumekumbatia sera ya kutovumilia ufisadi wowote na tumedhamiria kuitekeleza bila uoga au upendeleo.”
Ili kuhakikisha uadilifu unadumishwa katika idara ya mahakama, Jaji Mkuu alitangaza kuzinduliwa kwa kamati za maadili katika vituo vyote vya mahakama kote nchini.
Kamati hizo zitawajumuisha majaji, maafisa wa mahakama, mawakili na wawakilishi wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) miongoni mwa washikadau wengine.
Wote hao watashirikiana kupiga ripoti juu ya masuala yanayopaswa kuangaziwa na wakati huohuo kushughulikia tabia zinazokiuka maadili.