Mgombea wa wadhifa wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC Raila Odinga kesho Ijumaa ataelezea maono na masuala atakayoyapa kipaumbele ikiwa atachaguliwa kwenye wadhifa huo.
Raila ataelezea maono yake wakati wa mkutano utakaoandaliwa katika ukumbi wa Umoja wa Afrika, AU mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
“Mkutano wa Addis Ababa utakuwa jukwaa la kuzindia maono na vipaumbele na mpango tekelezi ili kuangazia changamoto zinazolikabili bara la Afrika, kwa kutumia fursa zilizopo na zinazochipukia barani humo, kwa muktadha wa Ajenda ya AU ya mwaka 2063,” umesema Ubalozi wa Kenya nchini Ethiopia katika taarifa.
Mkutano huo utawaleta pamoja wawakilishi kutoka nchi wanachama wa AU, jumuiya za kiuchumi za kikanda, viongozi wa biashara, vijana, wawakilishi wa wanawake na mashirika ya kijamii.
Raila anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mohamoud Ali Youssou na Mawaziri wa zamani wa Mambo ya Nje Anil Gayan (Mauritius) na Richard Randriamandrato (Madagascar) katika azima yake ya kutwaa wadhifa huo.
Uchaguzi wa kumtafuta mrithi wa Moussa Faki Mahamat kutoka Chad umepangwa kuandaliwa mwezi Februari mwakani wakati wa mkutano wa AU.