Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga amekutana na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir wakati akiimarisha kampeni zake za kutaka kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.
Wawili hao wamekutana mjini Juba huku Rais Kiir akiunga mkono azima ya Raila kutaka kumrithi Moussa Faki ambaye muhula wake wa kuhudumu unaelekea kumalizika.
“Nilikuwa na mkutano wenye tija mjini Juba na Rais wa Sudan Kusini. Asante, Mheshimiwa Salva Kiir Mayardit, kwa kunikaribisha. Unngaji mkono wako na dhamira ya kuichochea Jumuiya yote ya Afrika Mashariki, EAC kuniunga mkono kugombea uenyekiti wa AUC unathaminiwa sana,” alisema Raila baada ya mkutano huo.
Viongozi kadhaa wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC wameelezea kumuunga mkono Raila kuwania wadhifa huo.
Wao ni pamoja na Marais Yoweri Museveni wa Uganda, Samia Suluhu wa Tanzania na Paul Kagame.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu, Baraza Kuu la Umoja wa Afrika, AU liliidhinisha kwa kauli moja kuwa mwenyekiti mpya wa AUC atachaguliwa kutoka Afrika Mashriki.
Kufuatia uamuzi huo, Afrika Mashariki ilitakiwa kuwasilisha wagombea watakaowania wadhifa huo wakati wa uchaguzi utakaondaliwa mwezi Februari mwaka ujao.
Hadi kufikia sasa, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Somalia Fawzia Yusuf Adam ametangaza nia ya kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa AUC huku Djibouti pia ikiripotiwa kumsimamisha mgombea.