Chama cha UDA kimeahirisha awamu ya tatu ya marudio ya uchaguzi wake wa mashinani uliopangwa kufanyika Jumamosi, Machi 7 mwaka huu.
Kwenye taarifa, mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya chama hicho Anthony Mwaura amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kifo cha mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno aliyefariki mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na ajali ya ndege.
Mwaura sasa anasema uchaguzi huo utafanyika Machi 14 ili kuwapa wanachama muda wa kutosha kuomboleza kifo cha mbunge huyo.
Awamu ya tatu ya marudio ya uchaguzi wa mashindani imeahirishwa katika kaunti za Meru, Tharaka Nithi, Embu, Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Samburu, Trans Nzoia, na Uasin Gishu.
Kaunti zingine ni Elgeyo Marakwet, Nandi, Baringo, Laikipia, Nakuru, Kericho, Bomet na Vihiga.
Kwa upande mwingine, awamu ya pili ya marudio ya uchaguzi imepangwa kuandaliwa Aprili 9 katika kaunti za Mombasa, Kwale, Kilifi, Tana River, Lamu, Taita Taveta, Garissa, Wajir, Mandera na Marsabit.
Kaunti zingine ni Isiolo, Kitui, Machakos, Makueni, Turkana, Kajiado, Bungoma, Siaya, Kisumu, Migori, Kisii, Nyamira na Kakamega.