Chama tawala cha United Democratic Alliance – UDA na Orange Democratic Movement -ODM vimefikia makubaliano ya kugawana maeneo ya kisiasa kabla ya chaguzi ndogo zijazo, hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wao wa kisiasa.
Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki, ametangaza kwamba vyama hivyo viwili vitaendesha kampeni za pamoja kuwaunga mkono wagombea wa serikali yao jumuishi katika chaguzi ndogo za ubunge wa maeneo saba zinazopangwa kufanyika tarehe 27 Novemba.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo mapya, UDA itawasilisha wagombea katika maeneo ya Mbeere Kaskazini, Banisa na Malava, pamoja na wadhifa wa Seneta katika kaunti ya Baringo.
ODM kwa upande wake itawasilisha wagombea katika maeneo ya Kasipul, Ugunja na Magarini.
Akizungumza wakati wa kutolewa kwa vyeti vya uteuzi kwa wagombea watatu wa ubunge kupitia UDA na wagombea 17 wa wadi, Profesa Kindiki alihimiza wagombea hao kushirikiana na wale waliowashinda katika mchujo wa chama ili kuhakikisha ushindi wa chama hicho.
Kindiki alisema kuwa serikali inaendelea na safari ya mageuzi ya kitaifa, akisisitiza kuwa utekelezaji kamili wa miradi inayoendelea kama ule wa makazi na huduma ya afya kwa wote utaacha athari ya kudumu katika maisha ya Wakenya.