UDA na ANC vyaungana rasmi kuwa chama kimoja

Chama kipya sasa kitajulikana kama United Democratic Alliance Party huku Issa Timamy akitajwa Naibu kiongozi wa chama, Kelvin Lunani ndiye Naibu mwenyekiti wakati Omboko Milemba akiwa Naibu Katibu Mkuu.

Martin Mwanje
2 Min Read

Hatimaye vyama vya UDA na ANC vimeungana rasmi kuwa chama kimoja kitakachofahamika kama United Democratic Alliance Party. 

Chama hicho kitabadilisha jina katika nembo yake kwani kinajumuisha alama za ANC kama vile picha na topografia na kitafanyiwa mabadiliko kadhaa katika uongozi wake siku zijazo.

Hayo yametangazwa na mwenyekiti wa UDA ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Embu Cecily Mbarire wakati wa hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Rais William Ruto na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Mbarire amewataka Wakenya kujiunga na chama hicho kipya akisema lengo lake ni kuwaunganisha Wakenya.

“Sisi kamwe siyo chama cha hisa. Hauhitaji cheti cha hisa ili kujiunga na chama hiki kipya ambacho tunakibuni leo,” alisema Mbarire wakati akihutubia waliohudhuria hafla hiyo.

“Sura yetu mpya ni sura ya Kenya iliyoungana ambapo kila Mkenya anapaswa kuwa mwanachama.”

Aidha, kufuatia kuungana rasmi kwa vyama hivyo na kuwa chama kimoja, maafisa kadhaa wapya wameteuliwa.

Wao ni Naibu kiongozi wa chama ambaye atakuwa Gavana wa Lamu Issa Timamy, Naibu mwenyekiti atakuwa Kelvin Lunani huku Naibu Katibu Mkuu wa chama akiwa mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba,

Maafisa wa sekretarieti wa ANC pia wataungana na wale wa UDA ili kukifanyia kazi chama kipya.

Ila kuna mambo kadha wa kadha ambayo bado hayajashughulikiwa.

Kutokana na hilo, kamati ya kushughulikia mambo hayo imebuniwa na ina kipindi cha miezi mitatu ijayo kuhakikisha utenda kazi wa chama kipya ni mufti.

 

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *