Chama cha UDA kitatangaza hivi karibuni hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga kwa kukejeli kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Gavana wa Embu, Cecily Mbarire wakati wa mkutano wa Magavana kutoka Mlima Kenya Mashariki uliofanyika huko Tharaka Nithi.
Magavana hao wakitumia mkutano huo kumshutumu Gavana Kahiga kuhusiana na kauli zake juu ya kifo cha Raila.
Kulingana na Magavana hao, kauli za Kahiga zilikuwa za kizembe na zisizostahili kutolewa na kiongozi wa hadhi yake.
Wakati huhuo, Magavana hao waliitetea serikali kuhusiana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika eneo hilo, na kupinga madai kuwa limetelekezwa wakati maeneo mengine yakipendelewa.
Magavana hao badala yake wametoa wito kwa utawala wa Kenya Kwanza kuongeza idadi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika eneo hilo.
Juzi Jumanne, Kahiga alinukuliwa kwenye video moja akionekana kufurahia kifo cha Raila kwa misingi kwamba miradi mingi ya maendeleo ilikuwa imeelekezwa eneo la Nyanza huku eneo la Mlima Kenya likitelekezwa.
Ni kauli ambazo zilikumbana na shutuma kali kutoka kila pembe na kumlazimu Kahiga kuomba msamaha familia ya Raila na Wakenya kwa jumla.
Ila, Kahiga amekana madai kuwa matamshi yake yalilenga kukejeli kifo cha Raila.
Shutuma dhidi yake zilimlazimu Gavana huyo wa Nyeri anayehudumu kwa muhula wa pili kuachia ngazi kama Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana.
Kunao wanaomtaka kuchukua hatua zaidi na kujiuzulu wadhifa wa Ugavana.
