Uchunguzi uliofanyiwa kichwa cha mwanafunzi wa chuo kikuu Rita Waeni Muendo, umebaini kuwa alinyongwa kabla ya kukatwa kichwa.
Mwanapatholojia Mkuu wa Serikali Johansen Oduor akizungumza na wanahabari siku ya Alhamisi, amesema kuwa kichwa cha mwanamke huyo kilikatwa katika kiwango cha shingo huku pia alama zilizokuwa katika fuvu zikiashiria kuwa aligongwa kichwani na silaha butu.
Pia kulikuwa na majeraha shingoni ya kuashiria kugongwa na kifaa butu.
Oduor alifanya upasuaji wa kichwa hicho kilichopatikana kimetupwa kwenye bwawa moja huko Kiambaa, baada ya familia ya marehemu kuthibitisha kuwa kichwa hicho kilikuwa cha Rita Waeni.
Mwili wa marehemu ulipatikana katika chumba kimoja cha kupangisha mtaani Roysambu kaunti ya Nairobi Januari 13.
Majasusi wamesema kuwa mauji hayo yalitokana na itikadi fulani zinazoendeshwa na baadhi ya watu humu nchini.
Mwili wa mwanafunzi huyo ulipatikana ukiwa umewekwa kwenye mfuko wa plastiki katika jaa la taka la chumba hicho lakini bila kichwa.
Washukiwa wawili wakuu wa muaji hayo wako gerezani huku pia kisu ,rununu sita ,tarakilishi tatu,laini 10 za simu kutoka mitandao tofauti na vifaa vingine vikipatikana katika chumba walimokuwa wakiishi washukiwa hao.