Mpango wa upasuaji na uchunguzi wa maiti 94 zilizofukuliwa kutoka msitu wa Shakahola umeanza leo Jumatatu.
Shughuli hiyo inaongozwa na Mkaguzi Mkuu wa maiti wa serikali Dr. Johansen Oduor.
Hii ni awamu ya tatu ya ukaguzi wa maiti tangu kuanza kwa mpango mzima wa ufukuzi katika msitu wa Shakahola.
Lengo lake ni kupunguza idadi kubwa ya miili iliyoko katika makafani ya hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.
Kufikia sasa, miili 336 imefukuliwa kutoka eneo hilo katika kile kinachochukuliwa kuwa mauaji ya halaiki.
Serikali imesimamisha kwa muda shughuli za ufukuaji hadi uchunguzi wa maiti hizo 94 ukamilike.
Wahasiriwa wanaaminika kuwa wafuasi wa mhubiri tata Paul Mackenzie aliyewashauri wafunge kula na kunywa ili wamwone Yesu.
Mhubiri huyo yuko rumande akisubiri kushtakiwa rasmi.
Upande wa mashtaka umeashiria kwamba huenda akashtakiwa kwa kosa la mauaji ya halaiki na mengine husika.
Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki amefichua kwamba bado kuna makaburi mengi ya pamoja katika shamba la Chakama.