Uchumi wa taifa hili unazidi kuimarika huku pato jumla la taifa la nchi hii, likiongezeka kwa asilimia 5.4 katika muda wa miezi sita iliyopita.
Akithibitisha kuwa uchumi wa taifa hili sasa ni dhabiti, Rais William Ruto alisema mfumko wa bei pia umepungua kutoka asilimia 9.2 mwaka jana hadi asilimia 5.4 mwaka huu.
Kiongozi wa taifa alisema kutokana na hayo, benki ya dunia imeorodhesha uchumi wa kenya kuwa wa 29 unaokuwa kwa kasi zaidi kote duniani.
” Kile ambacho tumetekeleza pamoja, juhudi tulizoweka pamoja na kujitolea kwetu, kumenusuru taifa hili dhidi ya janga la kiuchumi,” alisema Rais Ruto.
Akizungumza katika bustani ya Uhuru wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Kenya, Rais Ruto alisema serikali imetekeleza mbinu mwafaka za kubadilisha uchumi wa taifa hili.
Alisema taifa hili tayari limejinasua kutoka hatari ya madeni, na kwamba taifa hili limechukua mkondo ufaao.
“Nathibitisha kwamba taifa hili liko huru dhidi ya madeni na uchumi wa taifa hili ni dhabiti,” alihakikisha kiongozi wa taifa.