Shughuli ya kupiga kura imekamilika nchini Uruguay katika uchaguzi wa Urais ambao unaonekana kwenda kinyume na mtindo wa kawaida wa uchaguzi na wadadisi wanabashiri kwamba huenda ukaingia awamu ya pili.
Kinyang’anyiro hicho cha urais kinahusisha Yamandu Orsi, ambaye ni mwalimu wa Historia na meya wa zamani anayewakilisha chama Amplio na Alvaro Delgado wa chama cha Partido Nacional.
Kulingana na wadadisi awamu ya pili ya uchaguzi huo huenda ikaandaliwa Novemba 24 2024.
Orsi wa umri wa miaka 57, alijipatia asilimia 43.2 ya kura zilizopigwa huku Delgado wa miaka 55 akiwa na asilimia 28 ya kura kulingana na kampuni ya kura za maoni ya Equipos Consultores.
Wakili Andres Ojeda wa umri wa miaka 40 ni wa tatu akiwa amepata asilimia 15.5 hadi 16 ya kura kulingana na ubashiri huo ambao pia unaashiria kwamba hakunwa mwaniaji atatimiza zaidi ya asilimia 50 ya kura inavyohitajika.
Nchi hiyo yenye watu milioni 3.4 ilipigia kura ya kupunguza umri wa kustaafu hadi miaka 60 na kuondoa vikwazo kwa maafisa wa polisi wanaotekeleza misako katika makazi ya watu usiku.
Kura za maoni zinaashiria kwamba raia wa Uruguay walikataa mapendekezo hayo.
Watu nchini humo wanaonekana kufurahia utendakazi wa serikali huku rais Luis Lacalle Pou wa chama cha Partido Nacional akiungwa mkono kwa kiwango cha asilimia 50.
Serikali hiyo hata hivyo imejipata pagumu kujitetea kuhusiana na uhalifu uliokithiri hata baada ya kutatua tatizo la ukosefu wa ajira na mishahara.
Uhalifu unaoambatanishwa na ulanguzi wa dawa za kulevya ni tatizo katika nchi hiyo iliyo na pato jumla la taifa la kiwango cha juu ikilinganishwa na nchi zinazoizunguka.