Waziri mkuu mpya wa Canada Mark Carney amevunja bunge la nchi hiyo na hivyo kusababisha kuandaliwa kwa uchaguzi wa haraka, Aprili 28, 2025.
Hatua hiyo aliyotekeleza Jumapili na iliyokuwa ikitarajiwa na wengi, imeweka taifa hilo katika mfumo wa uchaguzi chini ya wiki mbili baada yake kuchukua wadhifa wa waziri mkuu kutoka kwa Justin Trudeau.
Inajiri pia wakati kuna mvutano kati ya nchi hiyo na Marekani.
Akizungumza na wanahabari baada ya kukutana na Gavana mkuu kuomba ruhusa ya kuvunja bunge, Carney alisema Canada inakabiliwa na wakati mgumu kufuatia hatua za kibiashara za Rais Donald Trump.
“Ninaomba watu wa canada mamlaka yenye nguvu na chanya ili kukabiliana na Rais Trump na kujenga uchumi mpya wa Canada ulio bora kwa kila mmoja kwa sababu najua tunahitaji mabadiliko.” alisema Carney.
Awali uchaguzi ulikuwa umepangiwa kuandaliwa Oktoba 20, 2025 lakini kulingana na wataalamu, Carney anatumai kwamba ukifanyika mapema utakuwa wa faida kwa chama cha Liberal, ambacho kinapendwa sana wakati huu.
Chama hicho kimeongoza Canada tangu mwaka 2015, na kimepata uungwaji mkono wa kiwango cha juu kufuatia hatua ya Justin Trudeau ya kutangaza kujiuzulu kwake kufuatia vitisho vya Trump.
Rais Trump wa Marekani aliweka viwango vya juu vya ushuru kwa bidhaa za Canada zinazouzwa nchini Marekani na amekuwa pia akipendekeza Canada kuwa sehemu ya Marekani.
Masuala hayo yameghadhabisha watu wengi nchini Canada ambao sasa wanaunga mkono serikali kwa dhati kutokana na msimamo wake kuhusu matendo ya Trump.