Walimu nchini Tanzania wameahidiwa mazuri na Coaster Jimmy Kibonde ambaye anagombea urais nchini humo kupitia chama cha MAKINI.
Kibonde alitoa ahadi hizo kwenye mkutano wa kampeni katika soko la Kilombero huko Arusha ambapo alisema kwamba iwapo atachaguliwa kuongoza Tanzania, ataboresha hadhi ya walimu.
Alisema atahakikisha kila mwalimu anapata vazi rasmi la kazi yaani suti na watakuwa wakitumia usafiri wa umma bila malipo.
Mwaniaji huyo wa Urais alielezea kwamba walimu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa la Tanzania ndiposa kila mwalimu atapatiwa suti tano.
Kulingana naye hiyo itakuwa ishara ya heshima kwa walimu kutokana na jukumu lao kubwa la kuelimisha jamii.
Kuhusu usafiri wa bure, Kibonde alisema serikali yake itashirikiana na wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha walimu hawatozwi nauli wanapokwenda au kutoka kazini, ili kuboresha mazingira ya kazi katika sekta ya elimu.
Haya yanajiri wakati ambapo kampeni za uchaguzi mkuu nchini Tanzania zinaingia kipindi cha lala salama kwani uchaguzi utaandaliwa Oktoba 29, 2025.
Mgombea mkuu wa urais ni Rais wa sasa samia Suluhu Hassan wa chama cha CCM. Aliyechukuliwa kuwa mpinzani wake mkuu wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu bado yuko kizuizini na huenda asishiriki uchaguzi.
