Uboreshaji wa kituo cha mpakani cha Suam waendelea

Naibu Rais Kithure Kindiki amezuru eneo hilo kujifahamisha kuhusu jinsi ujenzi wa kituo cha kisasa unaendelea.

Marion Bosire
1 Min Read

Naibu Rais Kithure Kindiki leo amezuru kituo cha mpakani cha Suam katika kaunti ya Trans Nzoia ambapo alikagua ujenzi unaoendelea wa kituo cha kisasa.

Ujenzi wa kituo hicho cha kisasa ni ishara ya kujitolea kwa Kenya kuimarisha na kurahisisha biashara, uunganishaji wa kikanda na uhusiano kati ya raia wa Kenya na Uganda nchi aliyoitaja kuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa Kenya.

Kituo cha Suam, kilicho katika eneo bunge la Endebess ni muhimu katika kuunganisha Kenya na Uganda na huwa kinashughulikia mpito wa watu wengi wanaotembea kwa miguu na hata wanaovuka kwa kutumia magari.

Kituo kipya kinachojengwa kitakapokamilika, kitatoa nafasi ya kufanyia kazi kwa maafisa wa forodha wa nchi zote mbili, hatua ambayo itarahisisha mchakato wa kuidhinisha bidhaa na watu na hivyo kupunguza msongamano.

Ziara ya Kindiki katika eneo hilo ni ufuatiliaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais ili kuhakikisha sehemu ya Kenya ya kituo kinachojengwa imekamilishwa haraka.

Naibu huyo wa Rais alisisitiza umuhimu wa kukamilisha kituo hicho na kuruhusu kazi zingine kuendelea kama vile ujenzi wa barabara ya kilomita 45, inayounganisha Suam na Kitale.

Kindiki alikuwa ameandamana na viongozi wengine akiwemo katibu wa usalama wa taifa na utawala Raymond Omolo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *