UASU yalaumu serikali kwa kutotii mapatano

Marion Bosire
1 Min Read
Constatine Wasonga, Katibu mkuu UASU

Katibu mkuu wa kitaifa wa chama cha wahadhiri wa vyuo vikuu nchini UASU Constantine Wasonga ameilaumu serikali kwa kutotekeleza yaliyomo kwenye mapatano yao.

Wasonga anasema hatua hiyo sasa imesababisha kulemazwa kwa shughuli za masomo katika vyuo vikuu kote nchini.

Alikuwa akizungumza leo wakati wa matembezi ya kwenda kuwasilisha malalamishi yao kwa waziri wa elimu na wizara ya fedha kuhusu mgomo wao unaoendelea.

Katibu huyo wa UASU anaitaka serikali kukoma kutishia wahadhiri akisema kwamba watarejea kazini iwapo mapatano kati yao na serikali yatatekelezwa.

Wahadhiri wa vyuo vikuu nchini wamegoma kwa mara ya pili mwaka huu wa 2024 wakidai kwamba serikali imekosa kutekeleza mapatano ya pamoja ya mwaka 2021 hadi 2025.

Yapata wiki moja iliyopita, wawakilishi wa wahadhiri hao walifika mbele ya kamati ya bunge kuhusu elimu ambapo walitakiwa kudhibitisha kwamba serikali ilitenga bilioni 4.3 kushughulikia matakwa yao.

Share This Article