Wizara ya Afya imepigwa jeki baada ya kupokea vifaa vya tekonolojia ya habari vitakavyosaidia katika uangalizi na ufuatiliaji wa magonjwa katika maeneo ya mpakani.
Vifaa hivyo vinajumuisha vipakatalishi, kompyuta na nyaya za upitishaji umeme miongoni mwa vingine.
Vimetolewa na Umoja wa Ulaya, EU na serikali ya Ujerumani kupitia kwa Wizara ya Ushirikiano na Maendeleo ya Kiuchumi (BMZ).
“Msaada huo ni sehemu ya suluhisho za kidijitali za EU kuimarisha mifumo ya uangalizi na ufuatiliaji ya ugonjwa wa virusi vya korona katika eneo la IGAD,” amesema Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni.
“Msaada huo ni hatua muhimu katika jitihada zetu za kuifanya kuwa ya kidijitali mifumo ya usimamizi wa taarifa za afya, mifumo ya maabara, na mifumo ya uangalizi katika vituo muhimu vya mpakani kwa mujibu wa ajenda ya serikali.”
Vifaa hivyo vitasambazwa katika maeneo muhimu ya mpakani ya Busia, Malaba, Mandera na Moyale.
Inatarajiwa kuwa vitasaidia kuwezesha mawasiliano murwa na ushirikishanaji wa taarifa kati ya maeneo ya mpakani na pia kuwezesha uitikiaji wa pamoja na ulioratibiwa wa matishio ya afya ya umma, ikiwa ni hatua muhimu katika azima ya serikali ya kutambua haraka na kudhibiti mlipuko wa magonjwa.