Bunge la Kitaifa limeahidi kuwapiga msasa vilivyo Mawaziri wote 20 walioteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri.
Ahadi hiyo imetolewa na kiongozi wa wengi katika bunge hilo Kimani Ichung’wah.
Wanachama wa kamati ya bunge hilo inayoshughulikia uteuzi walikutana leo Alhamisi kukubaliana juu ya kanuni za kufuatwa wakati wa mchakato wa usaili.
“Kabla ya usaili wa Mawaziri wateule, Kamati ya Uteuzi iliandaa mkutano kuratibu kanuni za uidhinishaji wa watu 20 walioteuliwa kuwa Mawaziri ambao majina yao yamewasilishwa bungeni,” alisema Ichung’wah ambaye pia ni mbunge wa Kikuyu.
“Tumejitokea kuwapigia msasa vilivyo watu wote watakaofika mbele ya kamati, na kuhakikisha mchakati huo unafanywa bila chuki, upendeleo au roho mbaya.”
Rais William Ruto amewatea watu 20 kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri.
Wao ni pamoja na:
- John Mbadi – Waziri wa Fedha
- Salim Mvurya – Waziri wa Biashara
- Rebecca Miano – Waziri wa Utalii
- Opiyo Wandayi – Waziri wa Nishati
- Kipchumba Murkomen – Waziri wa Masuala ya Vijana na Michezo
- Hassan Joho – Waziri wa Madini
- Dkt. Alfred Mutua – Waziri wa Leba
- Wycliffe Oparanya – Waziri wa Vyama vya Ushirika
- Justin Muturi – Waziri wa Utumishi wa Umma
- Stella Soi – Waziri wa Jinsia
- Prof. Kithure Kindiki – Waziri wa Usalama wa Kitaifa
- Aden Duale – Waziri wa Mazingira
- Debra Mlongo Barasa – Waziri wa Afya
- Davis Chirchir – Waziri wa Barabara na Uchukuzi
- Soipan Tuya – Waziri wa Ulinzi
- Eric Muga – Waziri wa Maji
- Julius Migosi – Waziri wa Elimu
- Alice Wahome – Waziri wa Ardhi
- Dkt. Margaret Ndung’u – Waziri wa Habari na Mawasiliano
- Dkt. Andrew Karanja – Waziri wa Kilimo
Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi pia anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje na hatahitaji kupigwa msasa kwani hakuwa miongoni mwa mawaziri waliofurushwa Baraza la Mawaziri la zamani lilipovunjwa.
Hadi kufikia sasa, ni nyadhifa mbili pekee za Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mwanasheria Mkuu ambazo hazijajazwa.