Baadhi ya wabunge waliotumuliwa na chama cha ODM jana Jumatano wameelezea imani yao kuwa watayapiku majaribu ya sasa na kuendelea kuwahudumia raia waliowachagua.
Isitoshe, Seneta wa kaunti ya Kisumu Profesa Tom Ojienda ameapa kuendelea kushirikiana na Rais William Ruto katika utendakazi wake.
“Chama changu leo (jana Jumatano) kimenifurusha kwa kufanya kazi na Rais William Ruto. Sitaomba msamaha na nitaendelea kufanya kazi na Rais,” alisema Prof. Ojienda punde baada ya kubainika ametimuliwa chamani.
Mbunge wa Lang’ata Felix Odiwuor aliamua kuzungumzia majaribu yanayomkumba kwa kurejelea Bibilia Takatifu.
“Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Na Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita uwezo wenu. Lakini mnapojaribiwa atawapa na njia ya kutokea ili mweze kustahimili,” alisema Odiwuor almaarufu Jalang’o wakati akinukuu kitabu cha 1 Wakorintho 10:13.
Kamati kuu ya chama cha ODM jana Alhamisi ilitangaza uamuzi wa kuwatimua wabunge watano ‘waasi’ kwa madai ya kukiuka itikadi za chama na utovu wa nidhamu.
Kando na Odiwuor na Prof. Ojienda, wabunge wengine waliofurushwa chamani ni pamoja na Elisha Odhiambo wa Gem, Gideon Ochanda wa Bondo na mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi.
Omondi tayari amekaidi akisema kamwe hataomba msamaha na pia hahitaji kutetea kiti chake kwa tiketi ya chama cha ODM ili kukihifadhi wakati wa uchaguzi wa mwaka 2027.