Tume ya filamu nchini yaandaa maonyesho katika kongamano la tabianchi

Marion Bosire
2 Min Read
Wajumbe wa kongamano la tabianchi wakitizama filamu Between The Rains

Filamu kwa jina “Between the Rains” inayohusu tabianchi, ilizinduliwa na kuonyeshwa kwa mara ya kwanza katika jumba la KICC katika kongamano linaloendelea la Afrika kuhusu tabianchi.

Akizungumza kwenye maonyesho hayo ya Jumatatu jioni, mkurugenzi mtendaji wa ume ya filamu nchini Bwana Timothy Owase alisema mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa kwa jamii ulimwenguni kote huku madhara yake yakisababisha hasara kubwa kiuchumina hivyo kuna hoja kwamba hadithi tunazoonyesha zinafaa kudhihirisha tulivyoathirika na mabadiliko hayo.

Alisema filamu za matukio halisi yaani “Documentaries” huonyesha hali halisi kwa njia iliyo bora na hivyo zinatekeleza jukumu muhimu katika kutoa habari kuhusu matatizo ya ulimwengi na haja ya kuyatatua kama vile tatizo la tabianchi.

Owase alisema kwamba uundaji wa filamu za mabadiliko ya tabianchi unaweza kuletea jamii husika mapato kupitia ushirikiano na wanasayansi, mashirika ya kutunza mazingira na waundaji filamu ili kuhakikisha tasnia endelevu ambayo kando na kuhifadhi turathi asilia inatoa nafasi za ajira na kuwezesha utalii.

Between the Rains ni filamu ya matukio halisi ambayo iliandaliwa kwa muda wa miaka minne inayohusu mtoto aliyejipata katika utamaduni asili ambao umeathirika pakubwa na mabadiliko ya tabianchi.

Wakati wa mvua ya kiwango cha chini katika eneo la kaskazini la Kenya, watu wa jamii ya Turkana hujipata kwenye mizozo kati ya jamii hasimu huku wanyamapori wakinyemelea mifugo wao.

Kolei, mvulana ambaye anafanya kazi ya kuchunga mifugo ambaye jina lake linamaanisha “anayeishi na mbuzi”, anajipata akitathmini upya njia yake ya maisha kama shujaa wa jamii pamoja na kufifia kwa utamaduni uliotoa mwelekeo wa maisha yake.

Filamu hii inaonyesha vitisho vinavyokumba jamii ya Turkana mojawapo ya jamii za kale kabisa nchini.

Usiku wa leo, tume ya filamu imepanga maonyesho ya filamu tatu katika ukumbi wa KICC ambazo ni Boube of the Fulani, River Brown Water na Thank you For the Rain.

Share This Article