Serikali ya Kenya Kwanza inaunda sera na kuchukua hatua za kiutawala ili kuangazia changamoto zinazoibuka katika utekelazaji wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki anasema hatua hiyo inalenga kuhakikisha utekelezaji fanisi na endelevu wa mpango wa upatikanaji wa afya kwa wote nchini (UHC).
Kulingana naye, utoaji huduma bora, za gharama nafuu na zinazopatikana kwa wote ni moja ya hatua bora zaidi zinazochukuliwa na utawala wa sasa kuchochea mabadiliko ya kiuchumi humu nchini.
“Wizara ya Afya na washirika husika imepiga hatua katika mchakato wa kupitia upya kifaa cha upimaji wa mfumo huo ili kuhakikisha ni sahihi na hauna upendeleo kwa kujumuisha mrejesho kutoka kwa wananchi na washikadau wengine katika kipindi cha miezi mitano iliyopita,” alisema Naibu Rais.
Prof. Kindiki aliyasema hayo katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi leo Jumatatu alipoandaa Kongamano la Afya la Serikali Kuu na zile za Kaunti ili Kupitia Upya Utekelezaji wa UHC.
Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ahmed Abdullahi ni miongoni waliohudhuria kongamano hilo.
Mfumo wa SHA umekumbana na changamoto mbalimbali tangu kutekelezwa kwake mwaka jana huku Wakenya wakilalamikia kukosa huduma.
Hadi kufikia sasa, Wakenya milioni 19.5 wamejiandikisha kwa SHA.
Prof. Kindiki anasema serikali kuu na zile za kaunti zimedhamiria kuhakikisha kila Mkenya anapata bima ya afya ili kupokea matibabu bora na kwa kufanya hivyo kuhakikisha taifa hili lina watu wenye afya nzuri ya kuhuisha ustawi wake.