Tshisekedi aongoza kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini DRC

Marion Bosire
1 Min Read

Tume ya Uchaguzi nchini DRC inaendelea kutoa matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa Urais ambapo Rais Felix Tshisekedi anaongoza kwa kiwango kikubwa na anafuatwa na mwanabiashara Moise Katumbi.

Tshisekedi anaongoza kwa asilimia 81 huku Katumbi akiwa na asilimia 15.

Kulingana na tume hiyo ya uchaguzi, matokeo hayo ni ya kura milioni 1.9 huku wapiga kura waliosajiliwa nchini humo wakiwa milioni 44.

Tshisekedi wa umri wa miaka 60 amekuwa madarakani tangu mwaka 2019 na anatafuta kuhudumu kwa muhula wa pili wa miaka mitano.

Gavana wa zamani wa Jimbo la Katanga ambaye pia ni mwanabiashara Moise Katumbi wa umri wa miaka 58 ndiye wa pili huku Martin Fayulu wa umri wa miaka 67 akiwa wa tatu na asilimia 1.

Tshisekedi anashindana na wanasiasa wapatao 18 kwenye kinyang’anyiro hicho lakini wengi wao hawajatimiza hata asilimia moja ya kura ambazo zimehesabiwa kufikia sasa.

Share This Article