Rais Donald Trump wa Marekani amesitisha mahojiano ya wanaotuma maombi ya viza kuingia nchini humo katika balozi zake zote kote duniani katika juhudi za kukabiliana na wahamiaji haramu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ametangaza kuwa wizara hiyo imeanza kutoa mafunzo kwa maafisa wanaofanya kazi katika balozi zake kote ulimwenguni huku maombi ya mahojiano ya stakabadhi hiyo yakipangwa upya ili kutoa fursa kukamilika kwa mafunzo hayo.
Ingawa haijatajwa mafunzo hayo yanahusu nini, yamkini yanalenga kukaza kamba katika mchakato wa kuwasaili wanaotuma maombi ya viza huku takriban mataifa 75 yakilengwa.
Utawala wa Trump umekuwa ukipambana na idadi inayozidi kuongezeka ya wahamiaji haramu huku ukipata pingamizi kutoka kwa makundi ya kutetea haki za kibinadamu ambayo yanapinga sera zake za kuzuia hifadhi ya ukimbizi.