Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba mashambulizi dhidi ya Iran yataendelea hadi pale ambapo wataafikia malengo yao.
Aliongeza kwamba huenda wanajeshi wengi wa Marekani wakauawa kwenye mashambulizi hayo.
Trump alisema hayo kwenye video iliyochapishwa kwenye mtandao wake wa Truth Social jana Jumapili, ambapo alirejelea mashambulizi hayo kuwa “Operesheni ya haki”.
Aliongeza kuwa uchokozi huo dhidi ya Iran ni jibu kwa tishio la uendelevu wa Marekani kwani taifa la Iran lenye silaha za nyuklia na mizinga ni tishio kubwa kwa kila raia wa Marekani.
Matamshi sawia yalikuwa yametolewa na Trump na maafisa wakuu kwenye serikali yake, siku chache kabla ya mashambulizi ya Jumamosi alfajiri dhidi ya Iran.
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na maafisa kadhaa wakuu serikalini waliuawa kwenye shambulizi la Jumamosi.
Haya yanaendelea wakati ambapo Marekani na wandani wake kama Israel hawajathibitisha kwamba mizinga ya masafa marefu ya Iran ina uwezo wa kufika Marekani au iwapo imeunda silaha za nyuklia.
Iran imekuwa ikikanusha madai ya kutengeneza silaha za nyuklia ikielezea kwamba hata ingawa ingekuwa inafanya hivyo, mchakato mzima hugharimu miaka kadhaa na hazingekuwa tayari kufikia sasa.
Marekani inashirikiana na Israel katika kuishambulia Iran huku mazungumzo yakiendelea kati ya wawakilishi wa Iran na wale wa Marekani kuhusu silaha za nyuklia.
Trump alitangaza pia kuuawa kwa wanajeshi wapatao watatu katika mashambulizi hayo.
Alisema Marekani italipiza kisasi mauaji ya wanajeshi hao na kushambulia vibaya magaidi ambao anasema wanapinga vikali ustaarabu.