Travis Scott atatua baadhi ya kesi zilizotokana na tamasha la Astroworld

Marion Bosire
1 Min Read

Miaka karibia mitatu baada ya mkasa kwenye tamasha la Astroworld, mwanamuziki wa Houston Travis Scott ametatua na kumaliza kesi nyingi zilizotokana na tukio hilo.

Watu 10 walifariki kwenye mkasa huo huku wengine wengi wakiachwa na majeraha baada ya umati kusukumana kuelekea kwenye jukwaa mwaka 2021 na kusababisha mkanyagano.

Watu zaidi ya 300 waliokuwa wamemshtaki Scott wameafikia makubaliano na kumaliza kesi zao na kampuni ya Nation pamoja na mwanamuziki Scott.

Haijabainika walalamishi walilipwa fidia ya kiasi gani lakini bado kuna madai kadhaa mahakamani.

Stakabadhi za kesi hizo zinaonyesha kwamba wasiwasi wa usalama uliibuliwa kabla ya tamasha hilo. Waandalizi wanaripotiwa kutumiana jumbe za kusema kwamba hakukuwa na nafasi ya kutosha watu elfu 50 mbele ya jukwaa.

Wasiwasi huo unasemekana kunakiliwa kwenye ripoti za mkutano wa maandalizi baada ya tamasha la mwaka 2019 la Astroworld uliohusisha wahusika wakuu wa maandalizi ya awamu ya mwaka 2021 ya tamasha hilo.

Mawakili wa kundi lililosalia la walalamishi wanatarajiwa mahakamani wiki ijayo.

Share This Article