Mwanamuziki wa mtindo wa rap nchini Marekani Frazier Othel Thompson III, maarufu kama Trae Tha Truth amekutanishwa tena na binti yake ambaye alikuwa ametoweka kwa miezi kadhaa.
Kulingana naye, alipigiwa simu tarehe Mosi Januari 2025 na kufahamishwa kwamba aliyekuwa mke wake ambaye ni mama ya mtoto huyo wa miaka 6, alikuwa amekamatwa huko El Centro, California kwa madai ya kuhatarisha maisha ya mtoto huyo.
Alisafiri kwa ndege kuelekea San Diego kutoka Texas kisha akasafiri kwa gari umbali wa kilomita 160 hadi kwenye mji huo mdogo karibu na mpaka wa Mexico na Marekani ambapo alimpata binti yake aitwaye Truth.
Trae ameelezea pia kwamba mkewe wa zamani atahamishiwa Texas kushtakiwa huko.
Truth alikuwa amepotea kwa muda wa miezi minne huku Trae akielezea kwamba alikuwa amempeleka kwa mamake huko Houston mwezi Agosti, ambapo alistahili kukaa kwa siku mbili.
Mama huyo alikosa kurudisha mtoto kwa babake na tangu wakati huo amekuwa akihama hama naye akisaidiwa na nyanyake na wengine.
Mwanamuziki huyo alilazimika kutumia huduma za mpelelezi wa kibinafsi ambaye alimfuatilia mama mtoto hadi California, lakini akatoweka hadi alipokamatwa.