Tottenham Hotspur ilimaliza subira ya kukosa taji kwa miaka 17 baada ya kuwabwaga Manchester United bao moja kwa bila na kutwaa kombe la UEFA Europa League katika uwanja wa San Mamés mjini Bilbao, Uhispania, Jumatano usiku.
Timu zote mbili zilihitaji ushindi kwa udi na uvumba ili kufuzu kwa Kombel la Ligi ya Mabingwa msimu ujao; hata hivyo, kidosho bahati
akasimama na Spurs huku masaibu ya Man U almaarufu mashetani wekundu yakiendelea baada ya kunusurika kuenguliwa ligini msimu huu.
Mechi hiyo haikuwa na msisimko mkubwa ilivyotarajiwa huku Spurs wakipata bao kunako dakika ya 42 kupitia kwa Johnson na kudumu hadi kipenga cha mwisho.
Spurs walilinda bao hilo vilivyo katika kipindi cha pili na kujipatia hadhi ya taji la kwanza baada ya takriban miongo miwili.
Ushindi kwa Spurs uliacha kwikwikwi nyingi kwa wachezaji na mashabiki wa Mashetani wekundu ambao rekodi yao ya kucheza mehi 14 za kombe hilo bila kushindwa ilivunjwa kwenye fainali .