Mwanamuziki wa Canada anayeishi Marekani Tory Lanez atasomewa hukumu ya kesi aliyoshtakiwa na mwanamuziki mwenza Megan Thee Stallion mwezi Agosti. Jaji wa mahakama ya juu huko Los Angeles David Herriford alikubali ombi la kuahirisha hukumu hiyo hadi tarehe Agosti 7. Awali hukumu hiyo ilikuwa imepangiwa kutolewa Juni 13, 2023.
Waendesha mashtaka wanataka mwanamuziki huyo ahukumiwe kifungo cha miaka 13 gerezani huku Lanez akikabiliwa na uwezekano wa kurejeshwa nchini Canada.
Jaji Herriford aliamua kuwapa mawakili wa Lanez muda wa kutayarisha mapendekezo yao ya hukumu ambayo yanatarajiwa kuwasilishwa tarehe mosi Agosti. Jaji huyo awali alikataa ombi la mawakili wa Lanez la kuanza kesi hiyo upya.
Katika kikao cha mahakama cha muda mfupi Jumanne, Lanez alionekana akiwa ameinamisha kichwa na hakutaka kuangalia yeyote. Alikuwa amevaa sare za jela ambazo kwa kawaida huwa za rangi ya machungwa na kichwani akavaa kofia nyeusi.
Mwezi Disemba mwaka jana Lanez alipatikana na hatia kwenye makosa yote matatu ambayo ni, kuumiza mtu kwa kutumia silaha, kupatikana na silaha ambayo haikuwa imesajiliwa na kutoa silaha hiyo hadharani bila kujali.
Hata hivyo mawakili wa Lanez ambaye jina lake halisi ni Daystar Peterson, wanahisi kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kusababisha apatikane na hatia. Kulingana nao, ushahidi ambao ulitolewa mbele ya jopo la waamuzi haukustahili kukubaliwa na mahakama.
Megan Thee Stallion alitoa ushahidi mahakamani kuhusu kesi hiyo ambapo alielezea kwamba Lanez alimfyatulia risasi ambayo ilimuumiza kwenye upande wa nyuma wa mguu wake huku akimtaka acheze densi naye. Megan na Lanez walikuwa pamoja katika eneo la Hollywood Hills Julai, 2020 kisha wakaanza kuzozana baada ya Megan kudharau muziki wa Lanez.