Mwana kiungo wa kati wa Ujerumani na klabu ya Real Madrid Toni Kroos, ametangaza kustaafu baada ya kipute cha Euro cha mwezi Juni/Julai nchini mwake.
Chini ya Ujerumani, Gwiji huyo mwenye umri wa miaka 34, alishinda taji la Kombe la dunia nchini Brazil 2014.
Akiwa Bayern Munich, alinyakua mataji yafuatayo, klabu bingwa barani ulaya na dunia mara Moja kila Moja, kombe la Super la Ulaya, Bundesliga mara tatu sawia na lile la Ujerumani na pia akashinda mawili ya Super ya Ujerumani.
Alihamia Real Madrid ya Uhispania 2014 ambapo alishiriki mechi 463 na kuzoa mataji 22 yanayojumuisha: manne ya klabu bingwa Ulaya sawia na ligi mkuu-La Liga na lile la Super la Ulaya, matano ya klabu bingwa duniani na moja la Coper del Rey.
Kibinafsi, alitajwa mchezaji bora 2007 katika kombe la dunia la wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 nchini Korea Kusini.
Rais wa Real Madrid Florentino Pérez, amesema kuwa, ” Toni Kroos ni mchezaji wa haiba katika historia ya Real Madrid na hii klabu ni, na itakuwa nyumbani kwake”.
Kroos atachezea Real Madrid mechi ya mwisho Juni mosi kwenye fainali ya klabu bingwa barani Ulaya dhidi Dortmund ugani Wembley Uingereza.