Timu ya soka ya EAC yashinda timu ya kaunti ya Mombasa

Mechi hiyo katika uwanja wa KPA Mbaraki ilitizamwa na wageni kadhaa mashuhuri akiwemo Rais William Ruto huku wachezaji wakivumilia joto la hadi nyuzi 33 kuonyesha umahiri wao.

Marion Bosire
2 Min Read

Timu ya pamoja ya wabunge wa mabunge mbali mbali ya Jumuiya ya Afrika mashariki EAC iliishinda timu ya serikali ya kaunti ya Mombasa katika kinyang’anyiro cha soka katika michezo inayoendelea ya mabunge ya EAC jijini Mombasa.

Mechi hiyo katika uwanja wa KPA Mbaraki ilitizamwa na wageni kadhaa mashuhuri akiwemo Rais William Ruto huku wachezaji wakivumilia joto la hadi nyuzi 33 kuonyesha umahiri wao.

Mechi hiyo ilianza saa tisa alasiri na mbunge wa Mvita Machele Mohamed Soud wa timu ya EAC ndiye alifunga bao la kwanza baada ya kupatiwa pasi na mbunge wa Nyali Mohamed Ali, ambaye alikuwa ameingia uwanjani kama mchezaji wa akiba.

Jimmy Okwiri wa kaunti ya Mombasa alisawazisha na muda wa kawaida wa mechi ukakamilika na sare ya bao moja kwa moja ikabidi iamuliwe kwa penalti.

Timu ya EAC ilikamilisha kipindi cha penalti kwa ushindi wa mabao matano dhidi ya mabao manne ya timu ya kaunti ya Mombasa.

Kinyang’anyiro hicho kiliashiria moyo wa ushirikiano jambo ambalo michezo hiyo baina ya mabunge ya Afrika mashariki inajaribu kukuza.

Mchezo huo ulijiri saa chache baada ya ufunguzi rasmi wa michezo hiyo na Rais William Ruto katika bustani ya Mama Ngina Waterfront, na ulinuiwa kuanzisha michezo hiyo.

Leo, timu ya Kenya itatoana kijasho na mabingwa watetezi Uganda saa kumi alasiri.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *