Ilikuwa ni mbwembwe, shangwe, vifijo na nderemo pale timu ya taifa ya Morocco kwa chipukizi chini ya umri wa miaka 20 ilipowasili nyumbani mjini Rabat siku ya Jumatano, baaba ya kunyakua Kombe la Dunia.
Wachezaji waliokuwa juu ya mabasi walipokelewa na halaiki ya mashabiki walipowasili mjini Rabat kabla ya kukaribishwa rasmi katika Kasri la Mfalme na mwanawe Mfalme Mohammed wa sita.
Timu hiyo ilipoteza mchuano mmoja pekee huku ikiwalaza Argentina mabao 2-0 katika fainali ya Jumapili iliyopita nchini Chile, na kuwa taifa la pili kutoka Afrika kutwaa Kombe hilo baada ya Ghana mwaka 2009.