Tifa yamtaja Kithure Kindiki kuwa Waziri mchapa kazi zaidi

Tom Mathinji
1 Min Read

Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki, ametajwa Waziri mchapa kazi zaidi, katika utafiti wa hivi punde uliotolewa na kampuni ya Tifa.

Katika utafiti huo uliotolewa Jumatano, Seneta huyo wa zamani wa Tharaka Nithi, alipata asilimia 65.

Waziri mwenye mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa mambo ya nje, alikuwa wa pili kwa asilimia 62.

Waziri wa elimu Ezekiel Machogu, aliibuka wa tatu kwa asilimia 58 katika utafiti huo.

Waziri wa afya Susan Nakhumicha aliorodheshwa wa nne kwa asilimia 57, huku mwenzake wa uchukuzi na barabara Kipchumba Murkomen, akiibuka wa tano.

Katika utafiti huo uliofanywa kati ya tarehe 25 mwezi Novemba na tarehe saba mwezi Disemba mwaka 2023, mawaziri Kindiki na Murkomen walitajwa kuwa walioongoza kwa kuzuru kaunti nyingi.

Kwa upande mwingine Waziri Mudavadi, yule wa uchumi wa baharini  Salim Mvurya pamoja na Waziri wa michezo  Ababu Namwamba, wametajwa kuwa waliofanya safari nyingi za kigeni.

Share This Article