Wakenya wengi wanawaunga mkono vijana wa Gen Z, wanaoishinikiza serikali kufanya mabadiliko nchini. Hii ni kulingana na kura ya maoni iliyotekelezwa na kampuni ya utafiti ya Tifa.
Kampuni ya Tifa iliashiria kuwa asilimia 81 ya wakenya wanaunga mkono vijana wa Gen Z, huku wakikubaliana na maswala wanayoibua bila kuzingatia miegemeo yao ya kisiasa.
“Hatua ya kupunguza matumizi serikalini, ilikuwa shinikizo kuu kutoka kwa Gen Z ambayo wakenya wengi waliunga mkono,” ilisema Tifa.
Wakati huo huo, utafiti wa kura hiyo ya maoni, ulidokeza kuwa wakenya wengi waliowaunga mkono Gen Z, walipendelea zaidi maandamano ya mtandaoni.
Hatua ya Rais William Ruto ya kuvunja baraza la mawaziri, ilikaribishwa vyema na mamilioni ya wakenya, huku wengi wa waliounga mkono hatua hiyo wakiwa wafuasi wa muungano wa Kenya Kwanza.
Kulingana na kampuni hiyo, asilimia 67 ya wakenya waliunga mkono kutimuliwa kwa mawaziri, ishara kwamba wakenya wana hamu kubwa ya kufanywa mabadiliko serikalini.
“Hatua ya wafuasi wa Kenya Kwanza kuunga mkono kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri, ni ishara ya pengo kati ya utendakazi wa mawaziri na matarajio ya wafuasi wao wa kisiasa,” ilisema Tifa.
Aidha Tifa ilisema wakenya wengi wanapinga kurejeshwa serikali kwa mawaziri waliotimuliwa, ishara kuwa wakenya wanatarajia mabadiliko na uongozi mpya katika nyadhifa hizo.