The Ebonies watimiza miaka 47

Kundi hilo la uigizaji nchini Uganda, liliasisiwa mwaka 1977 na John W. Katende, mwandishi wa maigizo, mwelekezi, mtozi na mwigizaji.

Marion Bosire
2 Min Read

Kundi la uigizaji la ‘The Ebonies’ la Uganda limetimiza miaka 47 na lilisherehekea hatua hiyo muhimu katika hafla iliyoandaliwa kwenye hoteli ya Serena jijini Kampala.

Kumbukumbu zilitiririka pale ambapo wanachama wa sasa walipojumuika na wa awali huko wale ambao wametangulia mbele ya haki kama Dick Katende na Cissy Muwanga wakikumbukwa.

Wengi walisimulia wanayokumbuka tangu walipojiunga na kundi hilo la uigizaji lililodumu muda mrefu zaidi nchini Uganda.

Fauziah Nakiboneka mmoja wa wanachama maarufu wa kundi hilo amekuwepo kwa miaka 23 na anasema imekuwa kama shule ya kujifunza mambo mengi yanayohusu sio tu uigizaji bali pia maisha kwa jumla.

“Nimelelewa na kundi hili la Ebonies, limenifunza maadili, nimepata maadili mema ya kikazi na ujuzi katika uigizaji wa jukwaani na wa kunakiliwa kwenye video.” alisema Fauziah.

Huwa anaigiza kama ‘Sarah Gava’ na anasema uhusika huo umemfungulia milango na kumpa fursa nyingi tu ambazo zimechupisha tasnia yake.

Alikumbuka nyakati ambazo wangesafiri nje ya Uganda hadi maeneo kama London, Dubai na Marekani na ushirikiano na wanamuziki kama Jose Chameleon, Bobi wine, Catherine Kusasira, Ragga Dee na wengine katika maigizo yao.

Kwezi Kaganda Ruhinda alijiunga na kundi hilo mwaka 1989 na anashukuru kwa fursa nzuri iliyomwingiza katika uigizaji wa kitaaluma.

Kundi la The Ebonies liliasisiwa mwaka 1977 na John W. Katende, mwandishi wa maigizo, mwelekezi, mtozi na mwigizaji.

Wanapoendeleza sherehe za miaka 47, waigizaji hao wameandaa igizo la jukwaani kwa jina ‘Ebonies @ 47’ ambalo litaonyeshwa kesho Jumatano Januari Mosi 2025 saa moja jioni katika ukumbi wa Labonita.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *