Serikali ya Tanzania imekanusha madai ya wanavijiji kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kwa lazima kama sehemu ya mradi wa upanuzi wa hifadhi ya taifa kusini mwa nchi hiyo.
Siku ya Jumanne, Benki ya Dunia ilisema kuwa imesitisha ufadhili wake wa mradi wa utalii wa dola milioni150 katika Hifadhi ya Kitaifa ya Ruaha, ikisema ina wasiwasi mkubwa kuhusu madai hayo.
“Serikali ya Tanzania haikiuki haki za binadamu wakati wa kutekeleza miradi yake yote, ikiwa ni pamoja na hii inayofadhiliwa na Benki ya Dunia,” msemaji wa serikali Mobhare Matinyi aliiambia kituo cha shirika la utangazaji la serikali TBC.
“Kilichotokea ni kwamba Benki ya Dunia ilipokea baadhi ya ripoti kutoka kwa mashirika ya kiraia ambayo yalitilia shaka mradi huo, wakidai baadhi ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo hilo.
Taarifa hizo si za kweli.” Mradi huo unaojulikana kama Usimamizi Resilient wa Maliasili kwa Utalii na Ukuaji (Regrow), unalenga “kuboresha usimamizi wa maliasili na mali za utalii” kusini mwa Tanzania, Benki ya Dunia ilisema hapo awali.
Bw Matinyi aliambia gazeti la ndani kwamba Benki ya Dunia kufikia sasa imetoa dola milioni 125 ya ufadhili wake kwa Regrow, ambayo ilizinduliwa mwaka wa 2017.
Taasisi ya Taaluma ya Marekani ya Oakland iliripoti kwamba wanakijiji walibakwa na walinzi na walikuwa wakifukuzwa kutoka kwa ardhi yao kwa sababu hifadhi hiyo ilikuwa ikipanuliwa.
Taasisi ya Oakland pia ilidokeza ripoti, kutoka kwa mbunge wa Tanzania na shirika la jamii, kwamba walinzi walidaiwa kuwaua wanakijiji.