Tanzania imejikatia tiketi kwa fainali za 35 za kipute cha mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka ujao nchini Morocco kwa mara ya nne katika historia na ya pili kwa mpigo.
Hii ni baada ya kuwanyofoa tembo wa Guinea bao moja bila katika mchuano wa mwisho wa kufuzu wa kundi H Jumanne alasiri ugani Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Taifa Stars, wakicheza mbele ya lukuki ya mashabiki wa nyumbani, walicheza vyema kipindi cha kwanza wakimiliki mpira, ila walikuwa na amshambulizi butu huku kipindi cha kwanza kikiishia sare tasa.
Wenyeji waliongeza makali ya moto kwa mashambulizi kochokocho yaliyozaa matunda kunako dakika ya 61, baada ya mshambulizi Saimon Msuva aliyeunganisha pasi murua yake Abass Mudathir Yahya na kuwanyanyua mashabiki wa nyumbani.
Taifa Stars walijihami hadi kipenga cha mwisho na kusajili ushindi uliowafuzisha kwa fainali za pili mtawalia katika kipute cha AFCON kwa mara ya kwanza, baada ya kushiriki makala ya mwaka huu nchini Ivory Coast.
Taifa Stars walifuzu kwa AFCON kwa mara ya kwanza mwaka 1980, kabla ya kurejea tena mwaka 2019 nchini Misri na mwaka huu kwa mara ya tatu.
Tanzania wanajiunga na waandalizi wenza wa fainali za AFCON mwaka 2027, Uganda Cranes, ambao wamefuzu huku Kenya ikiwa mwenyeji mwenza pekee kufungiwa nje ya safari ya Morocco mwaka ujao.
Morocco itaandaa kipute cha AFCON cha makala ya 35 kati ya Disemba 21 mwaka ujao na Januari 18 mwaka 2026.