Tamasha la kwanza la utafiti nchini kuzinduliwa rasmi Jumatano

Marion Bosire
1 Min Read

Hazina ya kitaifa ya utafiti na chama cha wanasayansi wa umri mdogo nchini zimeshirikiana kuandaa tamasha la kwanza la kitaifa la utafiti nchini.

Tamasha hilo litazinduliwa rasmi Jumatano Agosti 21, 2024 na mgeni rasmi atakuwa mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei huku balozi wa Uingereza nchini Neil Wigan akitoa hotuba rasmi.

Mada ya tamasha hilo linaloandaliwa Agosti 19 hadi 23, 2024 ni “ushirikiano wa utafiti na maendeleo ya kijamii na kiuchumi”.

Waandalizi wa tamasha hilo wamelitaja kuwa la kipekee na muhimu na litaonyesha mafanikio ya hazina ya kitaifa ya utafiti, kuanzisha ushirikiano na kutia motisha uvumbuzi wa siku za usoni utakaochochea maendeleo kitaifa.

Watu zaidi ya 100 wanatarajiwa kuonyesha kazi zao wakati wa tamasha hilo ili ziweze kuchukuliwa kwa matumizi na wadau wa sekta ya kibinafsi, wenye viwanda na wenye biashara ndogo na za kadri.

Mwishoni mwa tamasha hilo, tuzo zitatolewa kwa lengo la kutambua jukumu kubwa la utafiti katika kuandaa mustakabali wa nchi ya Kenya siku zijazo na kuimarisha malengo yake ya maendeleo.

Maonyesho ya saba ya kitaifa ya sayansi na teknolojia yataandaliwa pia kwenye tamasha hilo chini ya mada “Kuendeleza maamuzi endelevu kwa mabadiliko ya tabia nchi”.

Share This Article