Takwimu za makala ya 19 ya mashindano ya Riadha Duniani

Dismas Otuke
2 Min Read

Makala ya 19 ya mashindano ya Riadha Duniani yalikamilika jana Jumapili usiku mjini Budapest, Hungary yakiwashirikisha wanariadha 2,100 kutoka mataifa 195 walioshindana katika kipindi cha siku 9.

Mashabiki 400,000 walinunua tiketi za kutazama mashindano hayo kutoka mataifa 120.

Rekodi moja ya dunia ilivunjwa pamoja na rekodi moja pia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20.

Rekodi 7 za mashindano ya dunia zilivunjwa, rekodi nyingine 11 za maeneo zikaandikishwa pamoja na rekodi 73 za kitaifa.

Wanariadha watatu walinyakua dhahabu mbili, Faith Kipyegon katika mita 1,500 na mita 5,000, Noah Lyles wa Marekani katika mita 100 na 200.

Alvaro Martin na Maria Perez kutoka Uhispania pia walishinda dhahabu mbili kila mmoja katika mbio za matembezi kilomita 20 na kilomita 35.

Mataifa 23 yalishinda medali za dhahabu, matano kutoka Afrika yaliyokuwa na wanariadha 9 huku mataifa mengine 26 yakinyakua medali za fedha na mengine 24 yakinyakua medali za shaba.

Kwa jumla, mataifa 46 yalishinda medali ambapo pia kwa mara ya kwanza kulikuwa na medali zilizogawanywa kati ya wanariadha wawili.

Katie Moon wa Marekani na Nina Kennedy wa Australia waligawana nishani ya dhahabu ya kuruka kwa upote kwa wanawake wakati Chris Nilsen wa Marekani na  Kurtis Marschall wa Australia wakigawana nishani ya shaba ya kuruka kwa upote.

Letsile Tebogo aliandikisha historia kuwa mwanariadha wa kwanza wa kiume  kutoka Afrika kunyakua nishani katika mbio za mita 100 aliposhinda shaba.

Share This Article