Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini imesema kuwa sehemu mbalimbali za taifa hili zitashuhudia mvua kubwa huku Wakenya wakitakiwa kujihadhari na mafuriko.
Utabiri huo ambao utaanza Aprili 2-8 mwaka huu, unajiri siku chache baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha uharibifu mkubwa jijini Nairobi.
Katika taarifa iliyotiwa saini na mkurugenzi wa idara hiyo Dkt. David Gikungu, hali ya joto pia itashuhudiwa wakati wa usiku, ambapo kiwango cha joto kitazidi nyuzi 25 katika eneo la Pwani na Kaskazini Mashariki mwa nchi.
Hali hiyo ya joto pia itashuhudiwa katika kaunti za Turkana, Marsabit, Mandera, Wajir, Isiolo, Garissa, Tana River, Lamu, Kilifi, Mombasa, na Kwale.
Idara hiyo imesema kiwango cha joto katika kaunti hizo kitazidi nyuzi 30 wakati wa mchana na inawashauri wakazi wa maeneo hayo kunywa maji kwa wingi.
Kulingana na idara hiyo, nyanda za juu katikati mwa nchi, magharibi mwa Kenya, Rift Valley, nyanda za chini kusini mashariki mwa nchi, eneo la Pwani, kaskazini mashariki na kaskazini magharibi mwa nchi zitapokea mvua kubwa kuanzia kesho Jumanne hadi Jumatatu wiki ijayo.
Aidha upepo mkali unatarajiwa kuvuma kutoka Kusini kuelekea Magharibi na kutoka Kaskazini kuelekea Mashariki.